Papa Francisko: Sala kwa ajili ya kuombea maskini duniani!
cq5dam.thumbnail.cropped.750.422.jpeg

09/11/2019

Papa Francisko kabla ya Ibada ya Misa Takatifu Siku kuu ya Kutabarukiwa kwa Kanisa Kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Jimboni Roma, alipata nafasi ya kushiriki sala na wajumbe wa Mkondo wa “ATD Quarto Mondo” ulioanzishwa na Mtumishi wa Mungu Padre Joseph Wresinski (1917-1988) mbele jiwe la msingi kwa ajili ya kuwakumbuka waathirika wa umaskini sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa Kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano ndilo Makao makuu ya Jimbo kuu la Roma, ambalo, Baba Mtakatifu ndiye Askofu wake mkuu. Kumbe, hii pia ni alama ya utakatifu wa Kanisa, licha ya watoto wake, wakati mwingine, kuogelea katika dimbwi la dhambi na mauti. Hii ni changamoto na mwaliko wa kujenga Kanisa hai, yaani Jumuiya ya Kikristo inayokita mizizi ya imani, matumaini na mapendo yake kwenye msingi thabiti ambao ni Kristo Yesu mwenyewe! Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuanza kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu Siku kuu ya Kutabarukiwa kwa Kanisa Kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Jimbo kuu la Roma, alipata nafasi ya kushiriki sala na wajumbe wa Mkondo wa “ATD Quarto Mondo” ulioanzishwa na Mtumishi wa Mungu Padre Joseph Wresinski (1917-1988) mbele jiwe la msingi kwa ajili ya kuwakumbuka waathirika wa umaskini sehemu mbali mbali za dunia.

Mkondo huu ulianzishwa ili kujenga uchumi unaosimikwa katika utu na heshima ya binadamu, kwa kuzingatia mahitaji yake msingi. Ulipania kutoa sauti kwa watu wasiokuwa na sauti kutokana na sababu mbali mbali sanjari na kujifunga kibwewe ili kupambana na umaskini wa hali na mali, kama sehemu ya upyaisho na maboresho ya maisha ya watu. Jiwe hili la msingi liliwekwa kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano kunako tarehe 17 Oktoba 1987, kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea watu wanaosukumizwa kwenye baa la umaskini; watu ambao utu, heshima na haki zao msingi zinasiginwa na kwamba, hata watu hawa wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa, kwa sababu ni sehemu ya sura ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.

Ufunuo wa Uso wa Kristo Yesu kati ya watu wanaoteseka ni sehemu ya wito na dhamana yao. Baba Mtakatifu na wajumbe hao katika sala hiyo, wamekuwambuka na kuwaombea mamilioni ya watoto wanaoteseka na kufa kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha; vijana waliokata tamaa ya maisha kwa kukosa fursa za ajira; waamini wanaokosa wahudumu wa Injili kutokana na uhaba wa miito mitakatifu; wameombea: utu, heshima na haki msingi za binadamu pamoja na kuanza mchakato wa ujenzi wa dunia hii ili iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Mwishoni, wameombea ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu kwa wale wote wanaomkimbilia kwa imani na matumaini, ili waweze kupata amani na faraja katika maisha yao.

https://www.vaticannews.va/sw/pope/news/2019-11/papa-francisko-mkondo-atd-quarto-mondo-sala-maskini-duniani.html

Palavras-chave :